Wakulima wa mbaazi wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wamepata dhamana ya kuuza mbaazi kilo1,223,665, zenye thamani Zaidi ya bilioni 2.5 katika mnada wa pili wa mbaazi msimu wa 2023/2024.
Operesheni meneja Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU LTD), Ndg. Marcelino Mrope amesema kwamba, tani 839 zenye thamani ya Zaidi ya shilingi bilioni 1.6 zilikusanywa katika mnada wa kwanza wa mbaazi kwa msimu huu. Ameyasema hayo wakati wa mkutano wa uuzaji wa mbaazi katika mnada wa pili Kijiji cha Msinji.
“Tulifanikiwa kukusanya tani 839 katika mnada wa kwanza wa mbaazi kwa msimu huu na kuuza mbaazi zetu kwa bei ya wastani shilingi 2,016 na kufanya zaidi ya shilingi bilioni 1.6 kuingia katika mzunguko wilaya ya tunduru”. Alisema
Katika mnada wa pili msimu huu wa mbaazi wanunuzi 15 wamejitokeza kuweka zabuni kununua mbaazi kilo 1,223,665, ambapo wanunuzi watano walifanikiwa kununua mbaazi zote zilizopo ghalani kwa bei ya juu shilingi 2,085 na bei ya chini shilingi 2,075 na kufanya bei wastani kuwa 2,079, ambapo jumla ya shilingi bilioni 2.5 zimeingia katika mzunguko wilaya ya Tunduru. Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika Tunduru (TAMCU LTD) Ndg. Mussa Manjaule wakati akitangaza bei ya mbaazi katika mnada wa pili wa mbaazi.
Aidha Ndg manjaule amewasihi wakulima wilaya ya Tunduru kuwa fedha hizi wanazozipata waendelee kuwekeza katika sekta ya kilimo kwa kuwa kilimo ni muhimili muhimu wa uchumi katika wilaya yetu ya Tunduru na kuwaomba kuendelea kulima Zaidi mazao hayo mbadala ya uchumi.
“Fedha tunazozipata tukawekeze, sisi kama wakulima ili tufikie lengo la kupandisha uchumi wa wilaya yetu”
Mnada wa tatu wa zao la mbaazi katika wilaya ya Tunduru unatarajiwa kufanyika mnamo Agosti 31,2023 katika Kijiji cha Angali .
Imeandaliwa na Orpa Kijanda,Kaimu Mkuu kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Afisa Elimu sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mwl. Patrick Haule ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule tano mpya kupitia programu ya uboreshaji wa Elimu Sekondari (SEQUIP).
Akizungumza ofisini kwake mjini Tunduru Afisa Elimu sekondari katika Wilaya ya Tunduru Mwl. Patrick Haule amesema katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa SEQUIP kwa mwaka wa fedha 2022/2023 serikali ya awamu ya sita ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 1.5 za ujenzi wa sekondari tatu mpya za kata ya Nakayaya, Majimaji na Lukumbule.
Shule zote za awamu ya kwanza ya programu hii zimekamilika na zimechukuwa wanafunzi wa kidato cha kwanza zaidi ya 500 katika shule zote tatu kwa mwaka huu.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Elimu Sekondari imepokea tena zaidi ya bilioni 1 kutoka serikali kupitia programu ya SEQUIP, ambapo shule mbili mpya toka kata ya Tinginya na Tuwemacho zitajengwa.
“Wanafunzi walikuwa wakitembea umbali zaidi ya kilomita 15 hadi 20 kutoka kata moja kwenda kusoma kata nyingine, hali iliyokuwa ilipelekea kuwepo kwa utoro mkubwa ambao ulisababisha wanafunzi wengi kuacha shule.”Alisema
Shule hizi za sekondari kupitia programu ya SEQUIP zitajengwa karibu na maeneo ya kuishi ili kuwawezesha wanafunzi kufika shule kwa wakati.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda,Kaimu Mkuu Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
23/08/2023.
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.