Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Mhe. Hairu Mussa, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa kupata hati safi ya ukaguzi wa hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Pongezi hizi zilitolewa katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani kwa kipindi cha robo ya tatu, kikao kilichofanyika mei 24, 2024.
Aidha, Mwenyekiti ametaja Mafanikio ya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ikiwemo kufikia lengo la ukusanyaji mapato hadi kufikia Asilimia 108, robo ya tatu, pia Kujenga soko la madini ya vito ambapo wanunuzi wote watakuwa wanafanya biashara katika eneo moja.
“Mafanikio haya katika Halmasahuri ya Wilaya ya Tunduru, yanatokana na juhudi zetu madiwani , tukishirikiana na Wataalamu wetu, kwahiyo tunatakiwa kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuwa na Maendeleo endelevu”.Alisema Mhe. Hauru.
Katika kikao hicho, wajumbe wa baraza walipokea taarifa mbalimbali kutoka kwa kamati za kudumu za halmashauri kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2024. Taarifa zilizowasilishwa ni pamoja na zile za Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, Kamati ya Huduma za Jamii, Kamati ya Ukimwi, na Kamati ya Maadili.
Afisa Serikali za Mitaa Mkoa wa Ruvuma, Ndg. Amandus Chilumba, pia aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa usimamizi bora wa ukusanyaji wa mapato. Aliwasisitiza wataalamu wa halmashauri kushirikiana vyema na madiwani ili kuhakikisha halmashauri inakuwa na maendeleo endelevu, hasa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Simon K. Chacha, aliwasilisha salamu za Serikali, ambapo Alisisitiza jukumu la madiwani kuwa mstari wa mbele katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao ya utawala.pia aliwataka madiwani kubuni vyanzo vingine vya mapato vitavyowezesha Halmashauri kuinuka Zaidi katika Maendeleo.
Aidha, aliwataka pia kusimamia na kuhakikisha kuwa wanafunzi wa shule wanapata chakula wanapokuwa shuleni, kwani hii itaboresha uwezo wao wa kujifunza.
Akifunga Kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mhe. Hairu Mussa amewapongeza Wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri kufikia Zaidi ya asilimia 100, amewataka wataalamu kuendelea kutekeleza majukumu yao ili Wilaya ya Tunduru iweze kusonga mbele kwa maendeleo.
Mafanikio haya ya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru yanaonyesha dhamira ya uongozi na wafanyakazi wake katika kuhakikisha matumizi bora ya fedha za serikali na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.